04 Mar 2025 / 76 views
McCarthy kuipeleka Kenya kombe la Dunia

Benni McCarthy amesema Kenya inaweza "kuwashangaza watu wengi" kwa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 baada ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa nchi hiyo.

Mchezaji huyo raia wa Afrika Kusini ametia saini mkataba wa miaka miwili ambao utamfanya kuwaongoza Harambee Stars hadi Fainali za Mataifa ya Afrika 2027 - mchuano ambao utafanyika katika ardhi ya nyumbani Afrika Mashariki, huku Kenya, Tanzania na Uganda wakiwa wenyeji pamoja.

McCarthy, 47, anachukua nafasi ya kocha wa muda Francis Kimanzi, ambaye amekuwa kocha tangu mkufunzi wa Uturuki Engin Firat ajiuzulu mwishoni mwa mwaka jana.

Mechi zake za kwanza zitakuwa za kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi huu ugenini nchini Gambia na nyumbani dhidi ya Gabon.

"Kushiriki Kombe la Dunia, ni moja ya hisia maalum zaidi ulimwenguni na ninataka kuwapa," McCarthy aliambia BBC Sport Africa.

"Kwa mawazo sahihi na kujitolea kutoka kwa wachezaji, na nia ya kujifunza na nia ya kutoa kila kitu walichonacho kwa kozi, nadhani tunaweza kushangaza watu wengi kwa kuendelea kufuzu kwa Kombe la Dunia."

Kwa sasa Kenya iko nafasi ya nne kati ya timu sita katika Kundi F ikiwa na pointi tano kutokana na michezo minne - pointi tano nyuma ya vinara Ivory Coast.

Ni washindi wa kundi pekee wanaofuzu kiotomatiki kwa mashindano hayo nchini Kanada, Mexico na Marekani. Washindi wanne bora kutoka kwa makundi tisa watapata nafasi ya pili kupitia mchujo.

McCarthy, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Afrika Kusini, aliwakilisha taifa lake kwenye Kombe la Dunia la 1998 na 2002, lakini Kenya haijawahi kufuzu kwa mashindano hayo.