28 Aug 2023 / 116 views
Kudus atua West Ham

Klabu ya West Ham imekamilisha usajili wa kiungo wa Ajax Mohammed Kudus kwa dau la £38m.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alifunga hat-trick katika ushindi wa Ajax katika mchujo wa kuwania kucheza Ligi ya Europa dhidi ya Ludogorets nchini Bulgaria siku ya Alhamisi.

"Nimekuwa na ndoto ya kucheza ligi kama hii tangu nikiwa mtoto," alisema Kudus, huku West Ham ikithibitisha kuwasili kwake Ligi Kuu. "Nina furaha sana kuwa hapa.

Lakini haiishii hapa, nataka kuendelea. Siwezi kusubiri kuanza." Atagharimu euro 44.5m pamoja na nyongeza na anafurahia matarajio ya soka ya kiwango cha juu nchini Uingereza.

"Ninajaribu niwezavyo kuwaburudisha mashabiki kwani nadhani hivyo ndivyo soka lilivyo," Kudus alisema. Brighton walifahamika kuwa wamefikia makubaliano na Ajax kwa Kudus mapema mwezi huu, lakini hawakuweza kukamilisha masharti ya kibinafsi.

Kudus alianza maisha yake ya soka katika klabu ya Nordsjaelland ya Denmark mwaka 2018, kabla ya kujiunga na Ajax mwaka 2020 ambapo amefunga mabao 27 katika mechi 87, na kuisaidia timu yake kutwaa mataji mawili ya ligi ya Uholanzi.

Kwa Ghana, Kudus amefunga mabao saba katika mechi 24 tangu aanze kucheza mechi yake ya kwanza mwaka 2019 na alianza mechi zote tatu kwa timu yake kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, akifunga mara mbili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Korea Kusini.

Ni mchezaji wa pili kusajiliwa na meneja wa West Ham David Moyes kutoka Ajax msimu huu wa joto kufuatia kuwasili kwa kiungo mwenza Edson Alvarez katika mkataba unaodhaniwa kuwa wa takriban pauni milioni 35.

West Ham pia ilisajili kiungo James Ward-Prowse kutoka Southampton na beki Konstantinos Mavropanos kutoka Stuttgart mapema mwezi huu.