18 Mar 2023 / 115 views
Alvarez asaini mkataba mpya

Mchezaji wa kimataifa wa Argentina, Julian Alvarez amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja katika klabu yake ya Manchester City ambapo mkataba wake huo utamuweka mpaka mwaka 2028.

Mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Argentina, fowadi huyo mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao 10 katika mechi 33 tangu ahamie kutoka River Plate msimu wa joto uliopita.

Alvarez alijiunga hapo awali kwa mkataba wa miaka mitano na nusu lakini sasa amesaini mkataba "ulioboreshwa" unaoangazia uchezaji wake katika klabu na nchi. Alisema City inampa "kila kitu anachohitaji" ili kufikia ubora wake.

"Kwa klabu kama City kuweka imani yao kwangu hivi ni ajabu," Alvarez alisema.

"Nimefurahishwa sana na msimu wangu wa kwanza hapa, lakini nina mengi zaidi ninaweza kufanya. Najua ninaweza kuwa bora zaidi, na City wananipa kila kitu ninachohitaji ili kutimiza uwezo wangu."

Alvarez aliifungia Argentina mabao manne nchini Qatar huku nchi hiyo ikishinda taji lake la tatu la Kombe la Dunia.

"Julian amevutia kila mtu katika Manchester City kwa uwezo wake wa kiufundi, ari na mtazamo," alisema mkurugenzi wa kandanda wa City Txiki Begiristain.

"Tuliona kwenye Kombe la Dunia jinsi alivyo na kipaji maalum. Kushinda kombe hilo katika umri wake ni jambo la kushangaza na sote tunajivunia kile alichofanikisha.

"Maendeleo yake hadi sasa yamekuwa mazuri sana, lakini sasa tunalenga kikamilifu kuendeleza mchezo wake hata zaidi na kumgeuza kuwa mmoja wa washambuliaji bora katika soka duniani."