24 Jun 2022 / 99 views
Lukaku arejea Inter Milan

Mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku amekamilisha dili la kurudi katika viunga vya klabu yake ya zamani ya Inter Milan kwa mkataba wa mkopo wa msimu mmoja.

Kiasi cha ada kinachodaiwa kulipwa na Inter Milan ni pauni milioni 8 ambapo Chelsea wanatajwa kutohusika tena na malipo ya mshahara wa Lukaku kwa msimu mzima.

Habari za ndani zinadai kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo ambaye ametangazwa rasmi kutimka klabuni hapo Bruce Buck pamoja na Mkurugenzi wa Utendaji mwanamama Marina Granovskaia walitaka kumbakiza Lukaku kwa msimu mmoja zaidi abaki klabuni hapo ili kuona ni kwa namna gani anaweza kurekebisha kiwango chake, lakini mmiliki mpya Todd Boehly alikuwa na mawazo tofauti na akaamua kumtoa kwa mkopo kurudi Inter Milan.

Kwa mujibu wa Matt Law ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Telegraph anadai hisia ndani ya klabu hiyo ni kwamba Romelu Lukaku anaweza kutolewa kwa mkopo wa msimu mwingine wa 2023/2024 au kuuzwa jumla.

Romelu Lukaku amekuwa na moja ya msimu wa kupanda na kushuka kwani alianza kwa kasi akifunga mabao matatu kwenye michezo miwili kabla ya kukubwa na majeraha pamoja na Covid-19 ambavyo vilimuondoa kwenye kiwango chake alichoanza nacho, amefanikiwa kufunga mabao 15 kwenye michezo 44 aliyocheza akiwa na uzi wa Chelsea huku mabao 8 kati ya hayo akifunga kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Uingereza.