19 Feb 2021 / 121 views
Yanga yapigwa faini

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya shilingi milioni moja baada ya mashabiki wa timu hiyo kutenda makosa mawili tofauti katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) baada ya kamati yake kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi.

Kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, mashabiki wa timu hiyo walionekana wamevaa vitambulisho wakimwaga vimiminika jambo lililoashiria imani za kishirikina.

Kwa kosa hilo Yanga wametozwa Sh laki tano, pia klabu hiyo imetozwa faini ya Sh laki tano katika mchezo dhidi ya Mbeya City kwa kosa la mashabiki wao kuzua ghasia kwa kuwarushia chupa waamuzi walipokuwa wakitoka uwanjani.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Februari 13, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Aidha, Polisi Tanzania imetozwa faini ya Sh laki tano kwa kosa la shabiki wa timu hiyo, Rashid Muninga ambaye ni askari polisi aliyevaa nguo za kiraia kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.

Naye kiongozi wa timu hiyo, Twahil Njoki amefungiwa kwa miezi minne na faini ya Sh laki tatu kwa kosa la kutukana waamuzi na kutishia kumpiga msimamizi wa Kituo cha Kagera.