24 Jun 2022 / 111 views
Madaktari nane kizimbani kifo cha Maradona

Madaktari wanane watafikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa makosa ya uzembe katika kifo cha mwanasoka maarufu wa Argentina Diego Maradona.

Jaji mmoja ameamuru kusikizwa kwa kesi ya mauaji ya bila kukusudia baada ya jopo la madaktari kubaini matibabu ya Maradona yalijaa "mapungufu na kasoro".

Maradona alikufa mnamo Novemba 2020 kwa mshtuko wa moyo huko Buenos Aires, mwenye umri wa miaka 60. Alikuwa akipata nafuu nyumbani kutokana na upasuaji wa kuganda kwa damu kwenye ubongo mapema mwezi huo.

Siku chache baada ya kifo chake waendesha mashtaka wa Argentina walianzisha uchunguzi kuhusu madaktari na wauguzi waliohusika katika uangalizi wake.

Mwaka jana, jopo la wataalam 20 walioteuliwa kuchunguza kifo chake liligundua timu ya matibabu ya Maradona ilifanya "njia isiyofaa, yenye upungufu na ya kutojali".

Pia ilihitimisha kuwa mwanasoka huyo "angekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuishi" kwa matibabu ya kutosha katika kituo cha matibabu kinachofaa, kulingana na uamuzi wa mahakama.

Miongoni mwa wanaokabiliwa na mashtaka ni daktari bingwa wa upasuaji wa neva na binafsi wa Maradona, Leopoldo Luque, daktari wa magonjwa ya akili na saikolojia, madaktari wawili, wauguzi wawili na bosi wao.

Wote wamekana kuhusika na kifo chake. Wote wanane watahukumiwa kwa ufafanuzi wa kisheria wa mauaji kulingana na uzembe uliofanywa huku wakijua kwamba inaweza kusababisha kifo cha mtu.

Uhalifu huo unaweza kushikilia kifungo cha miaka minane hadi 25 jela, kulingana na kanuni ya adhabu ya Argentina. Tarehe ya kesi bado haijawekwa.