14 May 2022 / 59 views
Bekham ataka Ronaldo abakie Man United

Klabu ya Manchester United wanatazamiwa kufanyiwa mabadiliko makubwa baada ya msimu huu lakini kiungo wa zamani David Beckham anatumai Cristiano Ronaldo atasalia kwa angalau mwaka mwingine.

Kipigo cha United cha 4-0 dhidi ya Brighton & Hove Albion mwishoni mwa juma kinamaanisha hawawezi kumaliza wakiwa juu zaidi ya nafasi ya sita.

Timu hiyo ya Old Trafford imemteua meneja wa Ajax Amsterdam Erik ten Hag kuchukua nafasi ya mkufunzi wa muda Ralf Rangnick kuanzia mwisho wa kampeni ya sasa, huku Mholanzi huyo akitarajiwa kukirekebisha kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu.

Ronaldo amefunga mabao 24 katika michuano yote msimu huu na Beckham, ambaye pia alivalia jezi nambari 7 ya United, anatumai fowadi huyo mwenye umri wa miaka 37 atasalia.

"Ni muhimu kwake - sote tunajua ni kiasi gani United ina maana kwake. Bado anafanya kile anachofanya vyema zaidi," Beckham aliambia Sky Sports kwenye Miami Grand Prix.

"Kufanya kile anachofanya katika umri wake ni ajabu sana kwa hivyo ni matumaini yetu kwamba itaendelea kwa mwaka mwingine au miwili."

Beckham, ambaye alishinda mataji sita ya Ligi Kuu akiwa na United, alisema mashabiki wamekwama kwenye nyakati ngumu, huku taji la mwisho la ligi kwa United likifika msimu wa 2012-2013.

"Imekuwa mwisho mgumu wa msimu. Lakini ni mwisho wa msimu, nina hakika mashabiki wengi wanashukuru hilo kwa sababu umekuwa mgumu - uliojaa heka heka," alisema.

"Wachezaji wamefanya kile ambacho wanaweza kufanya vizuri zaidi, na pia meneja. Nilifika uwanjani miezi michache nyuma na kila siti ilijaa kwa hiyo mashabiki bado wanaamini, wanaunga mkono, wanajitokeza kwa ajili ya timu.

"Ni kile ambacho mashabiki wa United hufanya. Hakuna timu nyingi ambazo zimepitia yale ambayo wamepitia katika miaka michache iliyopita na bado kujaza uwanja wao. Kutakuwa na mabadiliko."