24 Nov 2021 / 53 views
Ramos kuanza kuichezea PSG leo

Sergio Ramos huenda akacheza mechi yake ya kwanza akiwa na Paris St-Germain dhidi ya Manchester City. Ramos, 35, hajaichezea klabu yake mpya tangu alipoondoka Real Madrid msimu wa joto.

Amekuwa akiuguza jeraha la mguu lakini yumo kwenye kikosi kilichosafiri kwenda Manchester kwa pambano la uzani wa Kundi A.

City itatinga hatua ya mtoano iwapo itaepuka kushindwa.

Kikosi cha Pep Guardiola pia kitatinga hatua ya 16 bora ikiwa Club Bruges itashindwa kuifunga RB Leipzig katika mchezo mwingine wa Kundi A.

'Matokeo ya awali hayatakuwa na matokeo'

Mkufunzi wa PSG Mauricio Pochettino anawasili Manchester huku kukiwa na uvumi mwingi unaomhusisha na kibarua kilichoachwa wazi cha meneja katika klabu ya Manchester United.

Kocha wa zamani wa Tottenham, Pochettino aliiwezesha PSG kushinda 2-0 dhidi ya City kwenye Uwanja wa Parc des Princes mnamo Septemba, ingawa kundi hilo limebadilika na City sasa iko kileleni na kuhitaji pointi moja pekee kutoka kwa mechi yao ya pili ili kusonga mbele.

Pochettino pia alipanga ushindi wa Tottenham katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya City mnamo 2019.

Guardiola anasisitiza kwamba mikutano yake ya awali na Muargentina huyo haitakuwa na athari kwenye pambano hili la hivi punde.

"Ni tofauti kabisa - nchi tofauti, wachezaji, maumbo," alisema.

"Hata kwa meneja mmoja na timu moja kutoka mwaka mmoja inaweza kuwa tofauti - wachezaji wapya, mambo mengi yanaweza kutokea."