04 Mar 2021 / 160 views
Simba wawasili Sudan

Msafara wa wachezaji 25 wa Simba na viongozi saba umewasili salama nchini Sudan tayari kucheza mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh.

Simba inayoongoza Kundi A katika michuano hiyo ikiwa na pointi sita, inatarajiwa kuvaana na Al Merrikh keshokutwa Jumamosi.

Timu hiyo jana ilionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wakiwa na mafuta ya kupikia na maji ya kunywa waliyosafiri nayo ikiwa ni njia mojawapo ya kuepuka hujuma za wenyeji wao.

Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes, alisema kuwa maandalizi aliyoyafanya ya kikosi chake yanatosha kupata ushindi katika mchezo huo mgumu wa ugenini.

Gomes alisema kuwa anafahamu upungufu walionao wapinzani wao kutokana na kuwahi kukinoa kikosi hicho kabla ya kujiunga na Simba hivi karibuni.

Alisema kuwa katika mazoezi ya mwisho ya juzi Jumanne, ameona vijana wake wakifanya kwa morali kubwa katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.