20 Nov 2020 / 65 views
Msuva kuanza kikosi cha kwanza Wydad

Mshambuliaji mpya wa Wydad Casablanca, Simon Msuva amefunguka kwamba kucheza ligi ya nchi hiyo kwa muda mrefu pamoja na kuzoea lugha na chakula, vinamfanya ajione kwamba anaingia kwenye kikosi cha timu moja kwa moja.

Msuva ameongeza kwamba silaha hizo zitamfanya yeye aingie moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo mpya kwake kwa sababu itakuwa rahisi katika kufanya nao mawasiliano. Msuva hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka minne na nusu wa kujiunga na klabu hiyo ya Wydad Casablanca akitokea Difaa el Jadida ya nchini humo.

Nyota huyo anayeitumikia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa licha ya changamoto ya kuhamia kikosi kipya, anajiona anaweza kufanya vizuri na kupenya kikosi cha kwanza.

“Licha ya kwamba nimekuja kwenye klabu mpya lakini uzuri ni kwamba nimekaa hapa Morocco na naijua lugha pamoja na chakula pia nimekizoea.

“Hivyo naona kabisa naweza kufanya vizuri katika klabu hii mpya kwangu na pia wao wenyewe wananijua vizuri kwa sababu nimewafunga kwenye mechi kadhaa ambazo tulikutana nazo huko nyuma,” alimaliza Msuva.