16 Sep 2020 / 84 views
Messi atakiwa kupunguza mshahara

Klabu ya Barcelona itaanza kujadiliana na mshambuliaji wake Lionel Messi kupunguza mshahara wake kutokana na hali mbaya ya Kiuchumi kutokana na ugonjwa wa Corona.

Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu anatarajiwa kukutana na nahodha wa klabu hiyo, Lionel Messi ili kuzungumza juu ya uwezekano wa kukata mshahara wa nyota huyo kwa msimu ujao ikiwa ni mara ya kwanza tangu sakata la nyota huyo kutaka kuondoka Camp Nou.

Bartomeu atasimamia jukumu la klabu hiyo katika kupunguza gharama na atafanya mazungumzo na Messi pamoja na nyota wengine kwenye kikosi icho kukubali kukatwa mishahara.

Inaelezwa kuwa Barca ilipoteza zaidi ya € 98m ( kwa msimu wa 2019/20, ambapo hali ingeweza kuwa mbaya zaidi kama wasingemuuza kiungo Arthur Melo kwa € 72m kwenda Juventus.

Kwa hivyo ni lazima Barca kupunguza gharama na Bartomeu atalazimika kujadiliana na Messi, ambaye atawakilisha kikosi chote katika swala hilo yeye kama nahodha.

Messi na kikosi cha Barcelona walikubali kupunguzwa mshahara kwa 70% wakati wa janga la corona mwishoni mwa mwezi Machi.