16 Sep 2020 / 267 views
PSG kumsapoti Neymar suala la ubaguzi

Klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain imetoa tamko la kumuunga mkono mshambuliaji Neymar da Silva Santos Júnior, kufuatia tukio la kibaguzi analodaiwa kufanyiwa, wakati wa mchezo wa Ligi mwishoni mwa juma lililopita.

Mchezo huo ulioshuhudia Paris Saint Germain wakipepetana dhidi ya Olympic Marseille, uligubikwa na vurugu dakika mbili kabla ya kumalizika.

Chanzo cha vurugu hiyo ikitajwa ni rafu aliyochezewa mchezaji wa Marseille, iliyochagizwa na maneno ya kibaguzi kwa wachezaji wa timu pinzani.

Tukio hilo lilizua vurugu kubwa na kupelekea mwamuzi kutumia usaidizi wa VAR, na baadae kutoa adhabu ya kadi tano nyekundu.

Taarifa iliyotolewa na PSG kupitia kurasa za mitandao ya kijamii imeeleza kuwa: “Hakuna nafasi ya ubaguzi kwenye jamii, soka au maisha yetu.

Tunategemea kamati ya maadili kupitia LFP itafanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu sahihi. Klabu ipo tayari kushirikiana na LFP kama itahitajika.”