01 Aug 2020 / 69 views
Ake kutua Manchester City

Klabu ya Manchester City imetoa ofa ya paundi milioni 41 kwa ajili ya beki wa Bournemouth Nathan Ake ambapo ofa hiyo imekubaliwa.

Mazungumzo kati ya klabu hizo mbili juu ya uhamisho wa beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi yameanza kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa ligi kuu ya Uingereza lakini uthibitisho umekuja baada ya Bournemouth kushuka daraja.

Ake alijiunga na Bournemouth akitokea klabu ya Chelsea kwa usajili uliovunja rekodi ndani ya klabu hiyo ya paundi milioni 20 mwaka 2017 na amehusishwa kurudi Stamford Bridge lakini Manchester City wameingilia kati juu ya kumsajili mchezaji huyo.

Manchester City wamehusishwa na mabeki kadhaa kama Kalidou Koulibaly toka alivyoondoka Vincent Kompany mwisho wa msimu 2018-19 na walikosa kumsajili Harry Maguire ambaye amejiunga na mahasimu wao Manchester United.

Ake amecheza mechi 29 msimu huu wa ligi kuu soka nchini Uingereza akiwa na Bournemouth licha ya timu hiyo kushuka daraja.

Ada hiyo itaweka rekodi ya usajili kwa Bournemouth ambapo watapokea paundi milioni 41 kutoka kwa Manchester City kama dili hilo litakamilika.

Bournemouth wanaweza kuondokewa na wachezaji wake baada ya kushuka daraja ambapo wachezaji kama Callum Wilson na David Brooks wanatakiwa na badhi ya vilabu vya ligi kuu.

Usajili wa mchezaji huyo ukikamilika utakuwa usajili wa pili kwa Manchester City baada ya kumalizana na winga wa klabu ya Valenceia Ferran Torres.