14 Jan 2020 / 30 views
Reus amtabiria makubwa Haaland

Nahodha wa Dortmund, Marco Reus anaamini ujio wa Haaland katika kikosi hicho unaweza kuwa na faida kubwa kwa kuwa anafiti katika mfumo wa timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Robert Lewandowski.

Ni miaka sita sasa imepita tangu Lewandowski alipoondoka Dortmund kwenda Bayern Munich lakini kwa muda mrefu Dortmund wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata straika ambaye anaweza kufiti aina ya uchezaji wao kama ilivyokuwa kwa huyo waliyempoteza akaenda kwa wapinzani wao wa jadi, Bayern.

Baadhi ya mastraika waliofuata baada ya Lewandowiski kuondoka ni Adrian Ramos, Ciro Immobile na Michy Batshuayi lakini bado walishindwa kwenda sambamba na staili ya uchezaji ya Dortmund, hata ule uchezaji ambao ulikuwa ukipendelewa kutumiwa na kocha wao wa zamani, Jürgen Klopp nao ulipotea.

Marco Reus anaamini Bundesliga ambayo unaweza kuishuhudia kupitia king’amuzi cha StarTimes kwa kulipia kifurushi cha Uhuru kwa Sh 18,000 tu, inaweza kunogeshwa na Haaland kama ilivyokuwa enzi za Lewandowski alipokuwa Dortmund.

Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang aliyefunga mabao 98 katika Bundesliga akiwa Dortmund alikuwa mkali na bora lakini hakuwa akicheza katika aina ya uchezaji wa timu hiyo kwenye eneo la ushambuliaji.

Lewandowski akiwa Dortmund alikuwa ni mtu wa kati anayeweza kuwavuruga walinzi lakini Auba alikuwa akitokea pembeni na alisaidiwa na kasi yake, ndiyo maana alipata mabao mengi.

Reus anaamini sasa namba tisa mpya wa Dortmund anaweza kufiti vizuri katika mfumo wao kutokana na umbo lake, urefu, lakini tofauti yao kubwa labda ni katika namba ya jezi atakayovaa kwa kuwa ‘dogo’ mpya kwa sasa anavaa jezi namba 17 wakati mkongwe ambaye yupo Bayern alikuwa akivaa namba tisa.

Mfungaji huyo ni Aubameyang ambaye wao wenyewe wanakiri kuwa alikuwa mshambuliaji mzuri lakini mwenye staili tofauti ya uchezaji, alikuwa mfungaji bora wa ligi hiyo mwaka 2017.

Lakini tofauti na hapo, Dortmund wamekuwa wakipata wakati mgumu katika kufunga mabao mengi kwa kuwa hawajapata kile ambacho wamekuwa wakikihitaji.

Hata msimu huu napo wamekuwa na wakati mgumu, wameyumba kwa kiasi fulani, wanashika nafasi ya nne hadi sasa baada ya mechi 17, wakiwa wameshapotea mechi nne.