Messi anyakua Ballon d'Or ya sita
Mshambuliaji wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi amekuwa mchezaji wa kwanza kushinda Ballon d'Or mara sita baada ya jana kuwashinda Cristiano Ronaldo na Virgil Van Dijk.
Mchezaji huyo mwenye miaka 32 amenyakua tuzo hiyo baada ya kuikosa toka mwaka 2015 na hii ni kutokana na kuweza kufunga mara 54 katika klabu ya nchini kwake kwa mwaka 2018-19.
Virgil van Dijk alikuwa mshindi wa pili - yeye ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Liverpool katika saba bora, akiwemo Sadio Mane.
Mchezaji wa Juventus Cristiano Ronaldo, aliwahi kutunukiwa tuzo hiyo mara tano na amekuwa watatu katika kura.
Toka mwaka 2008 tuzo hiyo maarufu zaidi duniani imetawaliwa na wachezaji wawili ambao ni Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric aliingilia ufalme wa Messi na Ronaldo baada ya kushinda tuzo hiyo mwaka jana.
Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa mwaka huu kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo moja kwa pamoja.
Mara ya kwanza walikutana katika tuzo za mchezaji bora wa Ulaya (Uefa) mwezi Agosti ambapo Van Dijk aliibuka na ushindi wa tuzo hiyo. Mara ya pili wakaminyana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Fifa ambapo Messi aliibuka mshindi.
1. Leonel Messi (Barcelona na Argentina)
2. Virgil van Dijk (Liverpool na Uholanzi)
3. Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno)
4. Sadio Mane (Liverpool na Senegali)
5. Mohammed Salah (Liverpool na Misri)