02 Dec 2019 / 159 views
Mshindi wa Ballon d'Or kujulikana leo

Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2019 anatarajiwa kutangazwa leo usiku, na kwa mara nyengine tena kwa mwaka huu Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk watakuwa wanachuana vikali.

Kwa kipindi cha miaka 10, tokea 2008 mpaka 2017 tuzo hiyo maarufu zaidi ya wasakata kandanda duniani ilitawaliwa na washambuliaji hatari katika kizazi cha sasa Messi na Ronaldo, kila mmoja wao akishinda mara tano.

Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric alivunja ufalme wa Messi na Ronaldo baada ya kunyakua tuzo hiyo mwaka jana.

Mlinzi wa klabu ya Liverpool, Van Dijk ambaye ameshinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita anaonekana kutishia kuendeleza machungu kwa Ronaldo na Messi kwa mara ya pili mfululizo.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Messi Ronaldo na Van Dijk kukutana uso kwa uso katika kuwania tuzo kubwa mwaka huu.

Mara ya kwanza walikutana katika tuzo za mchezaji bora wa Ulaya Uefa mwezi Agosti ambapo Van Djk aliibuka na ushindi kwenye tuzo hiyo.

Mara ya pili wakaminyana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Fifa ambapo Messi aliibuka mshindi kwenye tuzo hiyo kubwa ya FIFA.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vikubwa barani Ulaya, kuna tetesi kuwa matokeo ya tuzo hizo yamevuja na kuonesha kuwa Messi ameshinda.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Messi anayecheza katika klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina amepata alama 446, akifuatiwa na Van Dijk mwenye alama 382.

Mshambuliaji wa Liverpool Mohammed Salah anatajwa kuwa katika nafasi ya tatu, Ronaldo nafasi ya nne huku mshambuliaji mwengine wa Liverpool Sadio Mane akaikamilisha tano bora kwa mwaka huu.