15 Nov 2019 / 41 views
Taifa Stars kushuka dimbani leo

Taifa Stars ya Tanzania inachuana na Equitorial Guinea leo jioni na mshambuaji wa taifa stars Mbwana Samatta amesema ana matarajio makubwa kuwa watakuwa na matokeo mazuri katika mechi hiyo.

Vijana hao wa Taifa Stars watatumia uwanja wa nyumbani kujaribu kupata alama zote kwenye mechi hiyo itakayoanza saa moja za usiku majira ya Afrika Mashariki jijini Dar es saalam.

Taifa stars ambao hawakushinda mechi yoyote katika fainali ya kombe la mataifa bingwa Africa AFCON zilizoandaliwa nchini Misri, wanamatarajio makubwa hasa baada ya mahasimu wao wa jadi Harambee Stars ya Kenya kutoka sare ya 1-1 na Misri huko Alexandria.

Kenya Harambee Stars iliandikisha matokeo hayo mema kuliko ilivyokuwa ikitarajiwa jana usiku ilipotoka nyuma na kusawazisha dhidi ya wenyeji Misri, katika mechi ya mkumbo wa kwanza ya kufuzu kwa michuano ya kuwania fainali ya kombe la mataifa bingwa barani Afrika ya mwaka wa 2021.

Mabingwa hawa mara saba wa kombe hilo walikosa huduma za nyota wao mahiri na mshambulizi matata wa Liverpool Mo Salah ambaye hakucheza kutokana na jeraha.

Wachezaji wengine wa Misri waliokosa mechi hiyo ni pamoja na kiungo wa kati Abdullah El Said ambaye pia anauguza jeraha.

Kutokuwepo kwao ilikuwa fursa kwa Harambee Stars ambao walilazimika kucheza mechi hiyo katika uwanja wa El Borg bila kubadilisha wechezaji kwani nafasi zao zilitumika mapema baada ya kipa Patrick Matasi kujeruhiwa kunako dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza na kisha kiungo Ayub Timbe kujeruhiwa.

Bao la Misri lilifungwa na Mahmoud Kahraba kunako dakika ya 42 ya kipindi cha kwanza baada ya mlinzi wa Gor Mahia Lawrence Juma kupeana pasi hafifu mno ambayo haikumfikia mlinda lango wa akiba Ian Otieno.

Mshambulizi matata wa Kenya Michael Olunga aliifungia Harambee stars bao la kusawazisha katika dakika ya 60 ya kipindi cha pili bao ambalo limeiweka Harambee Stars katika nafasi ya pili katika kundi G.