
Mchezaji apewa adhabu kwa kukosa penati
Mshambuliaji wa Club Brugge na timu ya taifa ya Senegal, Mbaye Diagne amekutana na adhabu ikiwa ni kuondoshwa kwenye kikosi na kulipa faini, sababu ikiwa ni kukosa mkwaju wa penati kwenye mechi waliyopoteza bao 1-0 dhidi ya Paris St-Germain.
Kocha wa Club Bruges Philippe Clement alielezea adhabu hiyo ni kwa sababu Hanas Vanaken ndiye aliyeteuliwa kuwa mpigaji penati wa timu na sio Diagne
Diagne aliyeingia kipindi cha pili cha mchezo alifanyiwa faulu iliyopelekea mkwaju wa Penati, na ikatokea kutoelewana juu ya nani apige na Diagne akapokonya mpira akapiga hata hivo ikaokolewa kwa urahisi na mlinda mlango wa PSG, Keylor Navas
"Hatakuwa kwenye uteuzi wangu wa mechi yetu ya ligi dhidi ya Antwerp, Jumapili" kocha Clement amesema katika mkutano na waandishi wa habari leo
"Na nitaamua katika wiki au miezi ijayo uwezekano wa kumrejesha kwenye timu. Pia kutakuwa na adhabu nzito ya kifedha"
Club Bruges kwa sasa ni ya tatu nyuma ya PSG na Real Madrid kwenye UCL Kundi A wakiwa na alama mbili tu lakini wanaongoza Msimamo wa Ligi Kuuu ya Ubelgiji.