09 Oct 2019 / 121 views
Ligi kuathiriwa na mfumo mpya wa UEFA

Ligi za soka maarufu duniani italazimika kupoteza nafasi moja kati ya nne za moja kwa moja kushirki michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Hiyo ni kutokana na mapendekezo mapya ya Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA juu ya kubadilisha muundo wa mashindano makubwa ngazi ya klabu barani humo pamoja na kutambulisha mashindano ya tatu ya vilabu.

Ligi hizo zitaathiriwa na mfumo huo, ambapo kuanzia msimu wa 2024 ligi hizo zitatoa nafasi tatu za moja kwa moja kuingia katika makundi ya Klabu Bingwa Ulaya na watakaoshika nafasi ya nne watalazimika kuanzia katika mchujo.

"Nafikiri ligi kubwa zitaridhia endapo sheria itatumika kwa kuzingatia usawa. Mfano ukitoa nafasi kwa EPL kuingiza timu nne halafu Bundesliga ukawatolea nafasi moja, lazima tatizo litatokea", amesema Lars-Christer Olsson ambaye ni Rais anayewakilisha ligi 36 za bara la Ulaya.

Jambo lingine ambalo linatarajiwa kuwekwa mezani ni kuhusu mgawanyo wa mapato kwa klabu ambazo hazishiriki michuano ya Ulaya, ambapo pendekezo lililopo ni la kuzipa mgawanyo hadi kufikia asilimia 25.

Wawakilishi wa ligi na mashindano mbalimbali ya Ulaya pamoja na klabu watakuwa na mkutano mwingine wa majadiliano mjini London wiki ijayo.