Solskjaer akubali kutupiwa lawama
Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema yupo tayari kupokea zigo la lawama baada ya juzi kikosi chake kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Newcastle United.
Mchezo huo ulikuwa wa tatu kupoteza kwa Manchester United tangu kuanza kwa msimu huu huku wakishinda michezo miwili na kutoa sare michezo mitatu na kuwafanya washike nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi baada ya kucheza michezo nane.
Solskjaer amekuweka wazi kuwa yupo tayari kutupiwa lawama kutokana na mwenendo wa timu hiyo, lakini anaamini mambo yatakuja kubadilika.
“Hakuna ambaye anafurahia mwenendo wa timu kwa sasa, najua kwenye mchezo huo dhidi ya Newcastle tuliwakosa baadhi ya wachezaji wangu, lakini hicho sio kigezo.
“Tumekuwa pamoja kama timu lakini tumeshindwa kuutawala mchezo na kupata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo kocha huyo aliongeza kwa kusema, kuna wakati wachezaji wake walionekana kama wametoka mapumziko ya timu za taifa.
“Kuna wakati wachezaji wangu walikuwa wanaonekana kama wametoka kwenye mapumziko ya timu za taifa, lakini lazima tuangalia nini kimetokea kwenye michezo yote nane ambayo tumecheza.
“Hakuna wa kulaumiwa mwingine ni mimi mwenyewe wa kutupiwa lawama, ninatakiwa kuhakikisha ninalimaliza tatizo hili. Kuna wachezaji wamekosa uzoefu, lakini ninaamini muda mfupi wale ambao wapo majeruhi watakuwa fiti na kuisaidia timu.