13 Aug 2019 / 23 views
Sneijder atundika daruga

Kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Wesley Sneijder ametangaza kustaafu soka kwa ujumla baada ya kucheza kwa miaka 17 ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Sneijder mwenye umri wa miaka 35 ameichezea timu yake ya taifa mechi 134 na kushinda magoli 31, ametangaza kustaafu soka kupitia Youtube chanel katika mji wake aliozaliwa wa Utrecht nchini Uholanzi na kutangaza rasmi kwasasa amestaafu kucheza mpira.

Sneijder ni miongoni mwa wachezaji waliofika fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 na kupoteza dhidi ya Uhispania kwenye mechi hiyo, pia ameshinda kombe la klabu bingwa na ligi kuu Seria A akiwa na Inter Milan, pamoja na ligi kuu ya La Liga akiwa Real Madrid.

Mchezaji huyo amecheza kwa mafanikio akiwa na Real Madrid, Inter Milan pamoja na Galatasaray huku klabu yake ya mwisho ikiwa ni Al Gharafa ya nchini Qatar ambapo ameichezea mpaka mwisho wa msimu wa mwaka wa jana.

Sneijder alianza kucheza soka katika academy ya Ajax na kupandishwa mpaka kucheza Ajax ya wakubwa mpaka alivyouzwa mwaka 2007 katika klabu ya Real Madrid nchini Uhispania na kufanikiwa kushinda kombe la La Liga.

Baada ya kucheza Real Madrid kwa mafanikio mchezaji huyo akajiunga na Inter Milan mwaka 2009 na kufanikiwa kushinda kombe la ligi kuu Italiano na klabu bingwa Ulaya chini ya kocha Jose Mourinho baada ya hapo akatimkia Galatasaray ya Uturuki.

Baada ya kucheza Galatasaray, mchezaji huyo akajiunga na klabu ya Nice inayoshiriki ligi kuu soka nchini Ufaransa Ligi 1 baada ya hapo akajiunga na klabu ya Gharafa ya nchini Qatar mpaka anatangaza kustaafu soka moja kwa moja.