13 Aug 2019 / 266 views
Alisson Becker kukaa nje wiki sita

Kipa wa Liverpool, Alisson Becker anategemea kukaa nje ya uwanja kwa wiki sita baada ya kuumia goti kwenye mechi ya kwanza ya ligi kuu soka nchini Uingereza dhidi ya Norwich.

Alisson ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Brazil alitolewa nje ya uwanja dakika ya 39 kwenye mechi hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na goli kipa mpya aliyesajiliwa kutoka Middlesbrogh, Andy Lonergan.

Alisson amekuwa tegemezi kwa Liverpool toka ajiunge na timu hiyo kutokea klabu ya AS Roma nchini Italia, ameisaidia Liverpool kushinda kombe la klabu bingwa barani Ulaya na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza msimu uliopita.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kuwa mchezaji huyo amepata jeraha kwenye goti na atakaa nje kwa wiki sita ili kupona kabisa na kurejea uwanjani.

Klopp amesema kuwa kutokuwepo kwa kipa huyo ni pengo kubwa sana kwao kutokana na ubora wake akiwa golini ila hakuna tatizo nafasi yake itachukuliwa na golikipa Andry pia kuna uwezekano wa kumrejesha kipa wao Karius aliyeko kwa mkopo Besktas.

Kocha huyo amesema kuwa kama timu inabidi wakabiliane na tatizo hilo kwani kipa huyo atakaa muda mrefu nje mpaka kurejea kwake kutakuwa na marekebisho kwenye mechi watakazocheza makipa wengine.

Liverpool kesho itashuka dimbani kupambana na Chelsea kwenye mechi ya Super Cup jijini Instanbull nchini Uturuki baada ya kushinda 4-1 dhidi ya Norwich kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi kuu soka nchini Uingereza.