12 Jul 2019 / 25 views
Tunisia yatinga nusu fainali

Timu ya taifa ya Tunisia imetinga nusu fainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika baada ya kushinda 3-0 dhidi ya Madagascar kwenye mechi ya robo fainali.

Tunisia imetinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15 kufanya hivyo kwenye michuano iliyofanyika nchini kwao mwaka 2004 na wakafanikiwa kutwaa taji hilo baada ya kuwafunga timu ya taifa ya Morocco kwenye mechi ya fainali.

Magoli ya Tunisia kwenye mechi hiyo yamefungwa na Ferjani Sassi aliyeshinda goli la kwanza baada ya kupiga shuti la mbali na kumgonga mchezaji wa Madagascar na kuingia golini na kuwandikia Tunisia goli la kwanza.

Youssef Msakni alishinda goli la pili dakika ya 60 huku goli la tatu na la mwisho likifungwa na mchezaji Naim Sliti dakika ya 90 ya mchezo huo.

Madagascar ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo ya mataifa ya Afrika na kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali baada ya kuwatoa timu ya taifa ya Congo kwa mikwaju ya penati kwenye mechi ya hatua ya 16 bora.

Baada ya ushindi huo, Tunisia itakutana na Senegal kwenye mechi ya nusu fainali itakayofanyika siku ya Jumapili huku Algeria ikikutana na Nigeria kwenye mechi kama hiyo baada ya kuwaondoa Ivory Coast.