11 Jul 2019 / 33 views
Samatta amwagia sifa Wanyama

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kwamba moja ya kumbukumbu nzuri alizoondoka nazo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Misri ni kukutana na Nahodha wa Kenya, Victor Wanyama.

Taifa Stars ya Samatta ilichapwa 3-2 na Harambee Stars ya Wanyama katika mchezo wa Kundi C Juni 27 Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo, Misri, lakini zote zikafungasha virago baada ya Raundi ya kwanza tu.

Samatta, mshambuliaji wa klabu ya KRC Genk Ubelgiji ameposti picha akiwa anawania mpira wa juu dhidi ya kiungo wa Tottenham Hotspur, Wanyama akiwa ameambatanisha na maelezo ya kumpa heshima mchezaji mwenzake huyo.

“Ilikuwa ni nafasi nzuri kucheza na mmoja wa wachezaji Bora na wa mfano wa kuigwa katika ukanda huu wa Africa mashariki, tunajivunia uwepo wako ndani ya East Africa Victor Wanyama,”.

Baada ya kufungwa mechi zote, 2-0 na Senegal, 3-2 na Kenya na 3-0 na Algeria, Taifa Stars iliondoka Misri bila hata pointi moja, ikishika mkia kwenye kundi hilo, nyuma ya jirani zao, Kenya waliovuna pointi tatu, huku Senegal iliyomaliza na pointi sita katika nafasi ya pili ikiungana na Algeria iliyokusanya pointi tisa kwenda hatua ya 16 Bora.

Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike imeshindwa kuvunja rekodi ya kikosi cha mwaka 1980 kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos, Nigeria ambacho angalau kiliambulia pointi moja baada ya sare na Ivory Coast ya 1-1, kikitoka kufungwa 2-1 na Misri na 3-1 na wenyeji, Nigeria.