11 Jul 2019 / 29 views
Gueye aipeleka Senegal nusu fainali

Timu ya taifa ya Senegal imetinga nusu fainali ya michuano ya Afcon baada ya kiungo wa timu hiyo Idrissa Gana Gueye kufunga goli la ushindi kwa timu hiyo.

Gueye alitamba na mpira na kumpigia pasi nyota wa Liverpool Sadio Mane ambaye hakuwa mchoyo akaamua kumrudishia ambapo mchezaji huyo alitupia wavuni.

Mfumo wa VAR ulitumika katika mechi za robo fainli ya michuano hiyo hivyo basi Mane alikuwa na magoli mawili ambayo yalikataliwa kwa kuotea.

Mchezaji wa Benin Olivier Verdon alipigwa kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo Gueye katika dakika za mwisho za mchezo huyo.

Benini ambayo ilitinga robo fainali bila ya kushinda mechi katika dakika 90 karibu ichukue uongozi baada ya masikhara ya mlinda lango Alfred Gomis.

Kipa huyo alishindwa kudhibiti pasi aliopigiwa na mchezaji mwenzake kabla ya mpira huo kutoka nje kwenye mechi hiyo ya robo fainali.

Baada ya ushindi huo sasa Senegal itakutana na mshindi kati ya Madagascar au Tunisia kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Misri kwasasa.