12 Jun 2019 / 135 views
Gervinho aachwa Ivory Coast

Mshambuliaji mkongwe wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Gervinho ameachwa kwenye kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya kombe la mataifa ya Afrika nchini Misri.

Gervinho mwenye umri wa miaka 32 anayechezea klabu ya Parma nchini Italia ameachwa kwenye kikosi hicho na kocha Ibrahim Kamara kwa ajili ya kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika yatakayoanza Juni 21 mwaka huu.

Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal na Roma ameshinda magoli 11 na kutoa pasi za mwisho 4 katika mechi alizocheza za ligi ya Italia msimu uliopita akiwa na Parma lakini hakujumuishwa kwenye kikosi hicho.

Kocha wa Ivory Coast, Ibrahim Kamara ameamua kumjumuisha kwenye kikosi hicho Nicolas Pepe anayechezea klabu ya Lile ambaye amekuwa mchezaji wa pili kwa ufungaji nyuma ya Kylian Mbappe wa PSG kwenye ligi ya Ufaransa Ligi 1.

Safu ya ushambuliaji ya Ivory Coast kwasasa inaongozwa na mchezaji wa Crystal Palace, Wilfried Zaha na Wilfried Bony ambapo walicheza kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Comoro ambapo walishinda 3-1.

Gervinho ameoneka kukasirishwa na kitendo hicho cha kuachwa kwenye kikosi hicho kwa ajili ya michuano ya mataifa ya Afrika yatakayoanza kutimua vumbi kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu.

Ivory Coast imepangwa kundi D kwenye michuano hiyo pamoja na timu za Namibia, Afrika Kusini na Morocco ndiyo kundi gumu kwenye michuano hiyo kutokana ubora wa timu hizo.